Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta ametoa rai kwa viongozi kujua namna bora ya kusimamia taratibu, sheria na kanuni zinazoongoza utendaji kazi wa mahali pa kazi wanaposimamia.
Mhe. Mugeta alitoa msisitizo huo jana tarehe 27 Machi, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha wakati akitoa mada kuhusu Usimamizi wa Nidhamu za Watumishi ambapo amesema pia ni muhimu Viongozi kufanya hivyo na kuwa vielelezo bora kwa watumishi walio chini yao kuhusu suala la usimamizi madhubuti wa nidhamu za watumishi wa Mahakama katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Ni vema kiongozi kusimamia taratibu za utendaji kazi, na kama wewe ni Kiongozi na unaingia ofisini asubuhi bila kuwa na kazi mahsusi za kufanya siku hiyo, huwezi kuwa kiongozi bora. Ni muhimu kama kiongozi uandae kazi zako siku moja kabla ili kazi utakazotekeleza zitokane na mipango uliyojiwekea,” alisisitiza Mhe. Mugeta.
Jaji Mugeta alisema kuwa, ni lazima viongozi wawe na utaratibu endelevu utakaowasaidia watumishi kuwa na mienendo inayofaa kazini. Watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa sababu ni wajibu wao, na si kwa sababu ya kumuogopa kiongozi wao.
Katika kikao hicho, yamejadiliwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya mashauri ambapo kwa kipindi cha kuanzia Oktoba, 2024 hadi Machi, 2025, Kanda ya Arusha kwa Mahakama za Wilaya, Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu zimepokea jumla ya mashauri 263, ambapo 214 yameamuliwa na yamebaki 362.
Aidha, hali ya mashauri katika Mahakama za Mwanzo Mkoa wa Arusha kwa mwezi Februari mwaka huu, jumla ya mashauri 1,831 yalisajiliwa na mashauri 2,075 yameamuliwa, yaliyobaki ni 1,229 na mashauri yaliyobaki mwezi Januari yalikuwa 1,473.
Vikao vya Menejimenti vya Kanda hujadili hali halisi ya utendaji kazi wa shughuli mbalimbali za Mahakama, ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto na mafanikio yaliyopatikana na kubadilishana uzoefu juu ya namna ya kuondoa changamoto zilizojitokeza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama mkoani Arusha wakiwemo Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Sophia Massati, Mtendaji, Bw. Festo Chonya, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Erasto Philly, Mahakimu Wakazi Wfawidhi wa Mahakama za Wilaya, Maafisa Tawala na Utumishi wa mkoani humo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)