tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
BARAZA LA WAFANYAKAZI LA KITUO JUMUISHI CHA MASUALA YA FAMILIA TEMEKE LAKETI
Post Media
post-media

Na NAOMI KITONKA, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke

Ikiwa ni miezi michache kuelekea sikukuu ya wafanyakazi Duniani, Baraza la Wafanyakazi la Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke limekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya wafanyakazi pamoja na jinsi yatakavyosaidia uboreshaji wa huduma za Mahakama.

Baraza hilo lilifanyika jana tarehe 27 Machi 2025 katika Ukumbi wa Mkutano na kuongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao cha Baraza hilo, Mhe. Mnyukwa alisema, “tunawashukuru kila mjumbe aliyepata nafasi na kuonesha utayari wa kuwepo mahali hapa ili kujadili mambo muhimu kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu hasa katika Mhimili huu wa Mahakama, sisi kama wawakilishi wa wafanyakazi tunao wajibu wa kuhakikisha wafanyakazi wanafurahia mazingira ya kazi kwa kupewa haki zao na maslahi yao pia kuboreshwa.”

Jaji Mnyukwa alisisitiza juu ya umuhimu wa vikao vya Mabaraza ya Wafanyakazi kwakuwa vinasaidia kuboresha mahusiano baina ya wafanyakazi katika majukumu ya utumishi pamoja na waajiri ikiwa ni pamoja na kupata matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa TUGHE kutoka Mahakama Kuu na Taifa, wajumbe walipata nafasi ya kujadili maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi na kufanya uchambuzi wa kina na maazimio yaliwekwa kwa ajili ya kuhakikisha hoja muhimu zinapatiwa majibu sahihi na ufumbuzi.

Wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mtendaji Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke, Bw. Samson Mashalla, Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi, Mjumbe wa TUGHE kutoka Taifa, Bi. Grace Magerezi, Mwenyekiti wa TUGHE kutoka Mahakama Kuu, Bi. Alice Haule, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Steven Wadi.

Wengine ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi IJC Temeke, Bi. Fatma Jumbe, Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi IJC Temeke, Bw. David Mbago, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mahakama ya Watoto pamoja na wajumbe wengine kutoka TUGHE.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)